Kuganda kwa asali (kunakojulikana kisayansi kama crystallization) ni mchakato wa asili kabisa na haimaanishi kuwa asali hiyo ni feki au imeharibika au imeongezwa sukari.
Asali asilia na mbichi huwa na mchanganyiko mkubwa wa sukari asilia na maji kidogo kitalamu asali huitwa super saturated solution. Sababu kuu zinazofanya asali igande ni kama ifuatavyo;
1. Kiwango cha Sukari ya Glucose:
Asali ina aina mbili kuu za sukari—yaani Glucose na Fructose. Sukari ya Glucose ndiyo inayosababisha asali igande.
Ikitokea glucose ni nyingi katika maua ambayo nyuki hukusanya malighafi za kutengenezea asali kuliko fructose- basi baada ya muda kidogo kupita mchakato ya kifizikia kutokea asali inaonesha matokeo ya kuganda….
Glucose inapojitenga na maji, hutengeneza chembechembe ndogo ngumu (crystals) zinazofanya asali ionekane kama imeganda au kuwa na muundo wa mchanga/mafuta ya mgando.
2. Hali ya Hewa na Joto:
Asali huwahi kuganda haraka zaidi inapowekwa kwenye mazingira yenye ubaridi (kama vile kwenye jokofu/friji). Hali hii pia ndio husababisha asali iliyo mikoa ya baridi kama vile njombe, iringa na kilimanjaro kuganda kwa haraka.
3. Aina ya Chombo cha Kuhifadhia:
Asali iliyohifadhiwa kwenye chombo cha plastiki huwa na tabia ya kuganda mapema zaidi kuliko ile iliyopo kwenye chupa ya kioo (glass).
4. Muda wa kukaa:
Kadiri asali inavyokaa muda mrefu bila kutumiwa, ndivyo inavyozidi kupoteza unyevu kidogo uliopo ndani yake kwa njia ya hewa (ikiwa chombo hakijafungwa vizuri), jambo linaloharakisha mgando.
5. Uchafu wa asili na Poleni (Pollen):
Asali mbichi ambayo haijachujwa sana kiwandani yaani kufanyiwa ultra Filtration inakuwa na vijidudu vya poleni, nta, na propolis. Vijidudu hivi vidogo vinafanya kazi kama kianzio au activators ambapo sukari ya glucose hujishika na kuanzisha mkachato wa kuganda (crystals).
6. Kiwango kidogo cha maji
Asali halisi ina kiwango kidogo sana cha maji (kawaida chini ya 18%). Kiwango hiki kidogo hakitoshi kuweka sukari yote katika hali ya kimiminika milele, hivyo sukari hujitenga na kuanza kutengeneza chembechembe ngumu. Kwa kuunganisha na sababu hapo juu
Ni muhimu kujua kuwa asali iliyochemshwa au kuchakachuliwa na sukari ya kiwandani mara nyingi hukaa muda mrefu sana bila kuganda kwa sababu virutubisho vyake vya asili vimeharibiwa. Kwa hiyo, kuganda ni ishara moja wapo ya kuonyesha kuwa asali yako ni mbichi na halisi.
Jinsi Ya Kuyeyusha Asali Iliyoganda:
Ikiwa unataka kuirudisha katika hali ya kimiminika, usiichemshe moja kwa moja jikoni kwani utaharibu virutubisho vyake. Badala yake, Chukua chupa ya asali au ndoo yenye asali iliyoganda na iweke ndani ya bakuli kubwa au sufuria au pipa lenye maji ya uvuguvugu au yanayojichemesha na joto lisilozidi degree centrigade 50. Iache humo kwa muda ikijiyeyusha yenyewe polepole.
Leave a Comment